Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hjaatul-Islam Sayyid Ali Fadhlullah, Imamu wa Ijumaa wa Beirut na mwanazuoni mashuhuri wa Lebanon, kutokana na mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Mtukufu Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), amewasilisha pongezi na salamu zake za heri, hususan kwa Waislamu, na kisha kwa Walebanon, pamoja na watu wote ambao nyoyo zao zimejaa mapenzi na huruma na wanaoishi kwa kuzingatia tunu za kibinadamu.
Alisema: “Tunawapongeza kwa mnasaba huu wa kuzaliwa Mtume ambaye Mwenyezi Mungu alimtuma akiwa ni rehema kwa walimwengu na ponyo la majeraha na maumivu yao. Tunatoa wito wa kufuata ujumbe wake katika njia ya kumuinua mwanadamu kuelekea katika kheri, haki, uadilifu na uhuru, pamoja na kushikamana na tunu za kimaadili na kibinadamu.”
Hujaatul-Islam Sayyid Ali Fadhlullah alisisitiza umuhimu wa kutumia uwezo wote na kuunganisha juhudi ili kukabiliana na changamoto na shinikizo ambazo nchi hii na watu wake wanakabiliwa nazo, kwa kuimarisha mazungumzo yanayounganisha watu na yenye msingi wa kitaifa, yaliyojaa busara na uwiano. Aidha, alitoa wito wa kuwaheshimu wengine na kufungua upeo wa mazungumzo nao, mbali na lugha ya kukata tamaa, mvutano na ubaguzi wa misimamo.
Alieleza matumaini yake kwamba nchi hii itapata amani, utulivu na kuwa salama, ardhi yake ikombolewe na wakazi wake warejee nchini mwao, ili Walebanon waishi pamoja katika nchi inayolinda heshima yao, kuhifadhi umoja wao na kuimarisha tunu za mapenzi, huruma na uadilifu.
Maoni yako